30 Juni 2025 - 13:43
Source: Parstoday
Human Rights Watch Ulaya-Mediterranean: Nchi zote zinapaswa kuchukua hatua kukomesha mauaji ya kimbari ya Gaza

Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu la Euro-Mediterranean Human Rights Watch limezitaka taasisi nchi zote zinazohusika kutekeleza wajibu wao wa kisheria na kimaadili na kuchukua hatua za haraka za kukomesha mauaji ya kimbari huko Gaza.

Taarifa ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu inasema: "Israel inazidisha mauaji yake ya kimbari huko Gaza katika kivuli cha ukimya usio na sababu wa jamii ya kimataifa."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Jeshi la Israel hivi karibuni limezidisha mashambulizi yake ya moja kwa moja na yaliyopangwa dhidi ya raia wa Palestina, likilenga zaidi makazi na kambi za wakimbizi."

Euro-Mediterranean Human Rights Watch imesema: Ndege za kivita za Israel zimefanya mfululizo wa mashambulizi makali ya anga siku ya Jumamosi kwenye maeneo ya makazi yenye watu wengi katika kitongoji cha Al-Tuffah, mashariki mwa Mji wa Gaza, na kusababisha mauaji ya raia kadhaa, wakiwemo watoto na wanawake.

Shirika la Kutetea Haki za Kibinadamu la Euro-Mediterania limeendelea kusema: Kuongezeka kwa mashambulizi ya Israel ni sehemu ya sera iliyopangwa ya kudhoofisha misingi ya maisha ya watu wa Gaza ikiwa ni sehemu ya kampeni ya mauaji ya kimbari yenye lengo la kuwafutuilia mbali Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirika hilo la kutetea haki za binadamu, ongezeko la mashambulizi ya Israel linashuhudiwa huku mauaji makubwa ya watu wenye njaa karibu na vituo vya kusambaza misaada vilivyowekwa na jeshi katikati na kusini mwa Ukanda wa Gaza, yakiendelea.

Taarifa hiyo inahitimisha kwa kutoa wito kwa nchi zote na taasisi zinazohusika kutekeleza wajibu wao wa kisheria na kimaadili na kuchukua hatua za haraka kukomesha mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Awali, Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ilikuwa imesisitiza kuwa, njaa inawaangamiza watoto wa Gaza na kutaka hatua za kimataifa zichukuliwe ili kukomesha jinai za Wazayuni.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha